Zebaki kama sabuni `kufua’dhahabu Mara - ISSRADHANS

Umoja na uzalendo

Umoja na uzalendo

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Wednesday 13 December 2017

Zebaki kama sabuni `kufua’dhahabu Mara





Image result for ZEBAKI
   .Wachimbaji wanena bila hofu: Eti kwao ni kawaida!
NA JAMES ZAKAYO, MARA
DALILI zinazoashiria ugonjwa wa saratani zimejitokeza miongoni mwa wachenjuaji wa dhahabu katika mgodi wa Kebaga, kata ya Kenyamanyori Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara kutokana na matumizi makubwa ya kemikali aina ya zebaki (mercury).
Lakini kushangaza baadhi ya wachenjuaji hao hawana hofu na hali hiyo wakisema kuwa ni sehemu ya maisha yao ingawa wataalamu wanasema ni hatari kwao.

Uchunguzi umebaini kuwa watu hao hutumia zebaki kuchenjua dhahabu kwa mikono jambo ambalo limewaathiri baadhi yao kubadilika rangi ya asili ya mwili ikiwa ni dalili mbaya.

Mwita Marwa ni mmoja wao, anapozungumza na mwandishi wetu anaonekana mwenye uso wa furaha katika kile anachokifanya licha ya kuwa haelewi kinachobadili rangi ya asili ya viganja vya mikono yake kuwa pinki.
 “Kubadilika kwa rangi ya mkono huu ni hali ya kawaida kwani ndio kazi zetu. Miaka yote wazee wetu wamechimba dhahabu na kuosha kwa kutumia kemikali hii lakini bado wapo,” anasema Marwa alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu hali hiyo. Hata hivyo anakanusha hali hiyo kusababishwa na matumizi ya zebaki, akidai hutokana na shughuli za uchimbaji za kila siku.
 Image result for ZEBAKI
Mchenjuaji mwingine mwanamke,  Motera Nyaseba anakiri kuwa wamewahi kutahadharishwa hatari ya matumizi ya zebaki ingawa  anadai kuwa wanalazimika kuitumia ili kupata pesa.
 “Sisi tunafanya hivi ili kuweza kutimiza haja za familia zetu kutokana na mzigo mkubwa wa sisi wanawake kuwa waangalizi wakubwa wa familia. Wengine hapa ni wajane. Pia sisi wanawake hatuna uwezo wa kuingia kwenye mashimo, hivyo wengi tumejikita hapa,”anasema Nyaseba.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Dk. Boniventure Bisulu anafafanua kuwa hali hiyo ni matokeo ya kuondoka kwa mafuta asili kwenye ngozi kutokana na watu hao kushika kemikali ya zebaki mara kwa mara.
 “Kemikali hii inapogusana na ngozi huingia mwilini kupitia matundu ya vinyweleo, huaribu seli na kisha kutengeneza saratani ya ngozi” alisema Dk. Bisulu.

Kutokana na shughuli  ya uchenjuaji kufanywa kila siku, pia madini hayo hupenya mwilini bila mtu kujua na kujikita ndani ya mfumo wa kutengeneza damu na kwenye mifupa kisha kuzuia utengenezaji wa damu  jambo ambalo husababisha upungufu wa damu (anemia).
“Kemikali hii inapokuwa inaendelea kushambulia sehemu ya kutengenezea damu,  baadae hutengeneza ugonjwa wa saratani ya damu ujulikanao kwa jina la kitalaamu la leukemia,” anasema Dk. Bisulu.
Zaidi, huharibu mfumo wa fahamu na kusababisha mtu kuwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu mara kwa mara (dementia), kukosa usingizi na misuli kuchoka.

Naye Dk. Innocent Kweka wa hospitali hapo, anasema zebaki ni moja ya kemikali zilizo katika kundi lijulikanalo kitalaamu kama in-organic  ambapo kundi la kemikali hizo zina madhara yanayofanana. Pamoja na saratani madhara mengine ni kuharibu mfumo wa fahamu ambao husababisha ugonjwa wa kutetemeka,  kupoteza kumbu kumbu na mengine.
“Hata hivyo madhara yake hutofautiana kulingana na kiwango kilichoingia mwilini. Jambo moja kubwa,  ifahamike kwamba zebaki ina tabia ya kushambulia seli  bila kujali kiwango,”anasisitiza Dk. Kweka.
Pia huweza kusababisha madhara kwa kunywa maji yenye viambata vya kemikali hiyo, ikigusa ngozi na kwa kuvuta puani ingawa dalili katika mfumo huo wakati mwingine hutofautiana, alisema.

Mkemia Rwige Ogunya wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa anakiri madhara yanayoelezwa na waganga hao na kuongeza kuwa, zebaki hushusha kinga ya mwili.
Ogunya anasema licha ya wachimbaji, wachenjuaji na jamii kuelimishwa mara kwa mara kuhusu madhara hayoi, baadhi yao wamekuwa wakaidi.
 “Wanatakiwa kufuata njia salama za kukamatia madini hayo kwa kutumia vifaa vya kuzuia au kupunguza madhara mwilini,”anasema Ogunya na kutaja vifaa hivyo kuwa ni vile vya kufunika mdomo, pua wakati wa kuchenjua, kujikinga na moshi wakati wa kuchoma dhahabu ili moshi wa zebaki usiwapate kwa namna yoyote.

Utafiti uliofanywa na kuandikwa katika jarida moja (sio Tanzania) liitwalo AMJ public health uliohusisha wachimbaji wadogo wa dhahabu huko mgodi wa Rwamagasa Geita hapa nchini ulieleza kuwa shughuli za wachimbaji wadogo wa madini hayo huongoza kwa matumizi ya zebaki.
Utafiti huo ulionesha kuwa watu milioni 80 hadi 100 kwenye nchi zinaoendelea ikiwamo Tanzania hutegemea uchimbaji wa madini. Kati yao,  milioni 13 hadi 15 huzalisha tani 500 mpaka 800 za dhahabu duniani kila mwaka.

Ili kupata tani hizo za dhahabu ni lazima tani 800 hadi 1,000 za zebaki zitumike jambo ambalo linatajwa kuwa ni chanzo kikubwa cha matatizo ya kiafya.

Naye Dk. Jonh Astete wa taasisi moja afya y nchini Peru anasema katika utafiti uliofanywa na taasisi yake ilibainika kuwa waathirika wakubwa wa zebaki ni watu wanaoishi pembezoni mwa migodi wengi wao wakijishughulisha na uchenjuaji wa dhahabu.

Utafiti huo ulihusisha watu 200 wanaozunguka maeneo ya mgodi katika mji wa Huepetuhe nchini humo na kuonekana kuwa ni rahisi kemikali hiyo kuenea kwa njia ya hewa na kudhuru maeneo ya jirani.

Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inasema limekuwa katika mapambano dhidi ya matumizi ya kemikali kwa kuzihamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Matifa kusimamia marufuku iliyowekwa, ingawa usimamizi wa sheria na marufuku hiyo ni kikwazo hasa katika nchi zinazoendelea.

Tanzania kupitia kamati ya Kitaifa ya Kimkakati (NAP) chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais ilitia saini mkataba wa Minamata nchini Japan  unaolenga kupunguza na kuondoa matumizi ya kemikali ya zebaki licha ya kemikali hiyo  kuendelea kuwepo  hapa nchini.

Taarifa ya wizara ya Nishati na Madini (sasa Madini) inasema kuwa Serikali imetambulisha kemikali ya Borax  kwa uchenjuaji wa dhahabu kama mbadala wa zebaki ingawa  baadhi ya wachenjuaji wamekuwa wakidai  kemikali hiyo haiwasaidii, kuendelea kutumia ile hatarishi.
Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, serikali imekusudia kutengeneza vituo maalumu vya kisasa ili kufundishia wachimbaji wadogo njia bora za uchenjuaji wa madini hayo bila madhara.

Ikumbukwe kuwa tukio kama hilo katika mgodi wa Kebaga liliwahi kutokea mwaka 2009 katika mgodi wa North mara uliopo Tarime kumwaga maji yenye kemikali katika mto Tigite na kusababisha athari za kiafya kwa binadamu na mifugo, ambapo watu kadhaa walipoteza maisha.

Mgodi wa Kebaga unategemewa na watu  kutoka  vijiji vya kata ya Kenyamanyori yenye watu 11,000 . Pia hutegemewa na  baadhi ya wanavijiji wa kata ya Turwa.
Baadhi ya dalili za mtu aliyeathiriwa na zebaki ni pamoja na ngozi ya mikono kuwa kavu na kubadilika rangi kuwa nyekundu, nyeusi ama pinki.

Zingine ni mwili kudhoofu, kukosa hamu ya kula, uoni hafifu, kupungua uzito, maumivu ya tumbo, kichefuchefu, kuvimba fizi na vidonda mdomoni.

Image result for ZEBAKI

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot