Hujafa hujaumbika, sikia kisa cha kijana huyu - ISSRADHANS

Umoja na uzalendo

Umoja na uzalendo

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday 12 December 2017

Hujafa hujaumbika, sikia kisa cha kijana huyu

NA MOHAMED NG'OULA

HUJAFA hujaumbika, msemo huu wa lugha ya Kiswahili unawiana na hali ya kijana, Joseph Chacha,  aliyezaliwa akiwa mzima mwenye kutembea kwa kutumia  miguu yake miwili, lakini leo hii amejikuta akihitaji msaada wa kutumia baiskeli ya walemavu kwa ajili  kumsaidia katika matembezi yake.


Kijana Chacha alizaliwa mwaka 1995 Bunda, mkoani Mara, ambapo mwaka 1998 alipata homa ya kichocho  na kumsababishia ulemavu wa kupooza viungo vyote mpaka hivi sasa.

Anasimulia kuwa umasikini wa kipato unao ikabili familia yake unamchango mkubwa katika ulemavu alionao, kwani kulikua na uwezekano mkubwa wa kupona nakumaliza tatizo hilo kama angepata matibabu stahiki.

“Magonjwa mengi nchi za Afrika yanasabisha kukwamisha ndoto za watu wengi hususan sisi masikini. Tatizo langu lilikuwa gumu na kuniathiri siku hadi siku kutokana na umasikini,  kama familia yangu ingekuwa na pesa basi ningepata matibabu yanayostahili,” anasema Chacha.

HARAKATI ZA MATIBABU
Katika mahojiano na mwanasafu wa kurasa hii (Tuishivyo), kijana huyo anaeleza baada ya kutokea kwa tukio hilo wazazi wake walimpeleka  Hospitali ya Wilaya ya Bunda ambako alipata matibabu, lakini hayakumsaidia, ndipo wakaamua kwenda kwa mganga wa  tiba za asili kwa ajili ya kupata matibabu lakini nako hakupata nafuu badala yake wakaamua kurudi nyumbani kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya kuendelea kupata matibabu.

“Nilipelekwa hospitali nikapata matibabu madaktari wakasema nina homa ya kichocho nikapata nafuu lakini baadae homa iliendelea ndipo wazazi wangu wakaamua kunipeleka kwenye tiba za asili homa ikaisha bali viungo vyangu vikaanza kushindwa kufanya kazi mpaka hivi sasa.”

HARAKATI ZA MAISHA
Pamoja na hali yake hiyo ya ulemavu, umasikini wa familia yake, kushindwa kumudu matibabu na mahitaji ya kila siku ya nyumbani kutokana kuishiwa kabisa pesa ya kupata mahitaji, alimuomba mama yake ampeleke katika shule za wanafunzi wenye ulemevu  ili ajue kusoma na kuandika kwa ajili ya kuendeleza ndoto zake.

Mwaka 2007  alipelekwa Shule ya Msingi Nyansror iliyopo Bunda ambako alijifunza  kusoma na kuandika lakini mwaka 2012 aliacha kusoma  akiwa darasa la tano kutokana na wazazi kushindwa kumudu gharama za mahitaji ya shule pamoja na kumwongoza kutokana na uzee.

“Sikupenda kuacha shule kwani nilikuwa na ndoto za kuendelea na shule ndio maana nilichelewa kuanza lakini nikaona bora nisome ili niweze kufanikisha malengo yangu, sikukata tamaa kwasababu ya hali  yangu ila ilinilazimu kuacha masomo baada ya mama yangu ambae ndio msaidizi wa maisha yangu kufariki, hapo ndipo ugumu wa maisha ulipoanza kutokana baba yangu alikuwa mzee pia alikuwa mlemavu wa mguu mmoja,” anasema.

CHANGA MOTO ZA MAISHA
Kijana Chacha anaeleza katika maisha yake amepitia changamoto nyingi sana, ikiwamo baada ya kufiwa na mama yake akanza kuombaomba misaada mbalimbali ikiwamo kanisani ili apate fedha kwa ajili ya kusukuma maisha yao. Anasema alipoona hali inazidi kuwa ngumu aliamua kwenda  kutafuta maisha jijini Dar es Salam.

Anasema alifika  Dar es Salaam mwaka 2012 na kuanza kuombaomba na kwamba  alipata changamoto mbalimbali ikiwamo kukoswa kugongwa na magari alipo kuwa barabarani, huku akilala na kuomba misaada stendi ya mabasi ya mikoani ya Ubungo.
Anasimulia kuwa alipatwa na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) hivi karibuni kutokana na kulala nje kila siku. 

WITO
Chacha anatoa rai kwa wanajamii wote wanaoguswa na changamoto zinazowakabili walemavu kumsaidia kwa kumchangia fedha  ili aweze kupanga na kuishi katika chumba chake na kupata mahitaji muhimu ya kila siku.

Aidha, anaiomba serikali na wadau mbalimbali kumuonea huruma na kumnunulia bajaji pamoja na kumpatia mtaji wa kufanyia biashara ili aweze kufanya biashara na kuendesha maisha yake.

“Nawaombe wadau mbalimbali na serikali  kunisaidia kupata mtaji ili nifanye biashara nijimudu kimaisha, Watanzania  wenzangu mimi sikupenda hii hali naumia kulala nje kila siku nalazimika kuishi barabarani sina pa kukaa, nakula kwa kutegemea wasamaria wema ambao wanafanyakazi maeneo hayo, pia namshukuru Mbunge wa Ubungo, Saidi kubenea, alinipatia baiskeli hii kipindi cha kampeni ingawa hivi sasa imeisha matairi yamepasuka kama unanyo yaona,” alisema Chacha kwa  huzuni kubwa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot