Mgagani: Ni Mboga, Kinga, Tiba, Sabuni, Mafuta na Mashudu - ISSRADHANS

Umoja na uzalendo

Umoja na uzalendo

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Thursday, 8 February 2018

Mgagani: Ni Mboga, Kinga, Tiba, Sabuni, Mafuta na Mashudu

NA ODRIAN NICOLAUS
LABLA kwa sababu ya ladha chungu ya mboga ya majani aina ya mgagani watu wengi hukimbilia kula mchicha na mboga zingine za majani ambazo hazina ladha hiyo.
Related image
Mmea wa mgagani  unavyoonekana  (pichani)
Ingawa wataalamu wanasema wanaofanya hivyo wanakimbia kinga na tiba ya maradhi mbalimbali, achilia mbali kwamba pamoja na kinga na tiba, mbegu na mizizi vinaweza kukamuliwa na kusafishwa kisha mbegu hizo  hutoa mafuta yanayotengeza sabuni, nishati ya bio-fuels na bidhaa zingine.

Mmea huo huota sehemu yoyote yenye udongo wa rutuba na tifutifu hasa kwenye mabonde, nyumba zilizohamwa (pagala) na maeneo mengine kama hayo. Bado inaaminika na wengi kuwa ni mboga ya watu masikini.
Ingawa kadri ya mahitaji ya tiba na lishe kila uchao, baadhi ya watu hasa katika ukanda wa Pwani wameanza kuchukua mbegu zake na kuzisia kama mchicha na mboga zingine za majani kwa ajili ya chakula, dawa, biashara ya kuchuuza na matumizi mengine.
ASILI YA MGAGANI:
Historia inaonyesha kwamba asili ya mmea wa mgagani ni Afrika Mashariki. Kutokana na mwingiliano wa watu, ndege na wayama ulienea hadi Ethiopia, Somalia, Asia Kusini na Amerika nazo kujumuishwa kama nchi zinazoasisi mmea huo.
Kwa mwingiliano huohuo, mmea huo uliendelea kusambaa katika nchi zote za kitropiki barani Afrika, Asia na Amerika kama anavyobainisha Dk. Edger Kapagi wa kliniki ya Mazingira Natural Products ya jijini  Mbeya.

Anasema ni mboga muhimu na inayothaminiwa mno na watu wa Bara la Asia (Wahindi na Wathai (Thailand) kutokana na watu wa jamii hizo kuwa kwanza duniani kutumia mmea hio kiafya ingawa asili  yake ni Afrika Mashariki ulikokuwa mboga zaidi.

Mgagani kama unavyotambulika kwa jina la kibotania,  cleome gynandra hujulikana na Waingereza kwa  majina ya African Cabbage, spider wisp, cats whisker, spider plants, na bastard mustards.

Huko Ufaransa, Wafaransa wanauita caya blanc, br’ede caya na mouzambe. Kiswahili jina maarufu ni mgagani ingawa yapo makabila kama vile wasambaa huuita mkabili shemsi na mwangani mgange.

Akizungumzia juu ya umuhimu wa mboga hiyo umesheheni virutubisho vingi na a madini ya beta carotene, vitamin C, Chuma, Magnesium, calcium na phosphorus, protini na amino acid nyingi, anasema Dk. Kapagi.

KUHUSU TIBA, KINGA:
Anasema ni kinga dhidi ya maradhi nyemelezi kwa watoto na watu wazima. Huukinga mwili na magonjwa ya kisukari, saratani na moyo, hutibu maumivu ya kichwa, kufunga choo, maumivu ya tumbo, kuzuia kutapika.

Zaidi;  anasema huzuia na kutibu homa ya naimonia (pneumonia),  maumivu ya sikio, bawasiri, maumivu ya hedhi kwa wanawake kwa ulaji wa mara kwa mara. Pia hutibu uvimbe katika kizazi cha mwanamke, jongo (gout) na anemia. 

“Mgagani unafaa kwa mama wajawazito wanaotaka kujifungua kwani huiandaa njia ya uzazi kupitisha mtoto na hivyo kumpunguzia maumivu mama husika (labor pains ) na kuongeza nguvu mwilini, kutoka maziwa kwa wingi, ya kutosha kwa mtoto kunyonya,”anasema na kuendelea...

Mizizi hutibu homa, kuumwa na n'ge na nyoka. Lakini ni mboga nzuri kwa waliotoka tohara kwani huongeza damu haraka iliyotoka wakati wa kutahiriwa. 
FAIDA ZA MGAGANI KIUCHUMI:
Mbegu zake zinaweza kukamuliwa na kusafishwa. Mafuta yake hutumika kutengeneza sabuni, bio-fuels na vitu vingine. Majani na mbegu ni chakula kizuri kwa ajili ya kuku na ndege wengine, ng’ombe, ngamia, farasi na wanyama wa porini wanaofugwa.

Ndiyo maana watu wengi wa ukanda wa Pwani ameanza kulima bustani za mmea wa mgagani na kuuza. Watu walioelekezwa matumizi yake wameanza kununua kwa wingi na kula kama mboga wakati huohuo kinga na tiba pia.

MATUMIZI:
Mkulima anaweza kumshauri mteja wake namna bora ya kupunguza uchungu wakati wa kuipika ili kumhamasisha mteja wake. Kutokana na lagha ya uchungu unaweza kumpoteza au kupunguza wateja, badala yake mlaji anashauriwa kuchanganya mgagani na tui la karanga ili kupunguza uchungu.

Kula kadri inavyofaa kama mboga zingine za mezani. Ni muhimu pia kuzingatia ushauri wa kitaalamu na kuanza kuchukulia mboga hii kama mkombozi wa afya, anasema Dk. Kapagi.

3 comments:

Post Top Ad

Your Ad Spot