Ulemavu si kigezo cha kukata tamaa - ISSRADHANS

Umoja na uzalendo

Umoja na uzalendo

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Wednesday 13 December 2017

Ulemavu si kigezo cha kukata tamaa


Kijana Mussa Shingano ambaye ni  mlemavu wa mguu   anayejishughulisha na shughuli za ujasiriamali  wa kuunga na kuchomea vifaa mbalimbali vya chuma akiwa katika moja ya vitanda anavyotengeneza , ofisini kwake  eneo la Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam. (PICHANI)

Na Mohamed Ng’oula
KATIKA kwenda sambamba na mikakati ya  nchi ya Tanzania ya viwanda, vijana wengi sasa wamekuwa wakichangamkia  fursa mbalimbali za kujiletea maendeleo kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Harakati hizo zimewasukuma vijana wengi  hata wenye ulemavu wa viungo kuacha kuombaomba na kujishughulisha katika shughuli za maendeleo.

Kwa bahati mbaya sana kuna baadhi ya vijana hususan wenye ulemavu bado wanajitenga katika kuchangamkia  fursa zilizopo kwa kujiona wao ni tofauti na watu wengine jambo linalo sababisha ongezeko la ombaomba nchini.
Hata hivyo, hali ni tofauti kwa kijana mlemavu, Mussa Shingano, ambaye katika kupambana na umasikini ameamua kupambana na hali yake hadi kufikia kuwa fundi wa kuchomea vifaa mbalimbali vya chuma.

Safu hii ya Tuishivyo, imemtembelea kijana huyo mwenye ulemavu wa miguu nyumbani kwake Gongo la Mboto, jijini Dar es salaam na kuzungumza nae masuala mbalimbali kuhusu harakati za maisha na namna anavyokabiliana na changamoto mbalimbali.
Shingano  anaeleza pamoja na hali aliyonayo hakuwahi kujiona yupo tofauti na binadamu wengine na anachofikilia  ni kufanya kazi kwa bidii ili afanikiwe katika maisha yake.

Kijana huyu aliyezaliwa mwaka 1992  mkoani Tanga, wilaya ya Pangani, katika kijiji cha Bushili anasimulia tangu alipozaliwa alipata ulemavu wa miguu yote miwili na jitihada mbalimbali za kumrudisha katika  hali ya kawaida zilishindikana na kujikuta akiwa alivyo hadi sasa.

“Nilizaliwa nikiwa mlemavu lakini kutokana na upendo wa mama yangu nilijiona mimi ni sawa na watu wengine, jamii haikunitenga  mpaka ikafika wakati nikamuomba mama anipeleke shule kwani  nilitamani kusoma nilipowaona wenzangu wakienda shule,” anasema Singano.

HARAKATI  ZA  MAISHA
Anasema mwaka 2000 alianza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Funguni na kumaliza elimu ya msingi 2007 na mwaka uliofuata alijiunga na elimu ya sekondari hapohapo Funguni na kuhitimu kidato cha nne 2011 ingawa hakubahatika kuendelea na masomo kutokana na matokeo yake hayakuridhisha.
“Sikukata tamaa baada ya kushindwa kuendelea na masomo nikamuomba mama yangu pamoja na majirani zangu msaada wa kwenda kusomea ufundi jijini Dar es Salam, niliomba mpaka ustawi wa jamii nikasaidiwa kusomeshwa ufundi wa kuunganisha vyuma chakavu,”  anasema Shingano.

MAISHA JIJINI DAR  ES  SALAAM
Anasimulia kuwa, pamoja na ulemavu alionao na umasikini wa familia yake hakutaka kuwa kuwa tegemezi au ombaomba kama walivyo baadhi ya watu wenye ulemavu.
Anasema alianza kusomea ufundi katika chuo cha ufundi cha watu wenye mahitaji maalumu kilichopo Yombo, jijini Dar es Salaam kwa muda wa miaka miwili akahitimu na kuanza kujishughurisha katika ujuzi wake huo mpaka hivi sasa.

“Nimemaliza elimu ya ufundi baada ya kuomba michango kwa watu mbalimbali na sasa nina ofisi yangu  ya kuchomea mageti, vitanda vya chuma na vifaa vya chuma maeneo ya Mombasa huko Gongo la Mboto, ingawa vifaa havijatimia lakini sio sawa na kuombaomba,” anasema.

CHNGA MOTO  ZA  MAISHA
Kama unavyo jua kila jambo lina changamoto zake, Singano anasimulia kuwa, tangu afariki baba yake mzazi akiwa darasa la kwanza, yeye alishikilia jukumu la kuwa kiongozi wa familia, hivyo wakati yupo shule anasoma pia alikuwa akimuhudumia mama yake mahitaji mbalimbali  kutokana na uzee alionao jukumu ambalo anaendelea nalo mpaka hivi sasa.
Hata hivyo, anasema pamoja na kufungua ofisi yake, vifaa alivyonavyo havikidhi mahitaji yake katika suala zima la kiufundi hali ambayo imekuwa ikimkwamisha kufanya kazi zake.

WITO

Singano anatoa rai kwa serikali na taasisi mbalimbali za kiraia  kumsaidia fedha zitakazomwezesha kununua vifaa ili aweze kupanua shughuli zake na kuajiri vijana wengine ili aepuke tabia ya kuombaomba na kuchangangia harakati za taifa za kujikwamua kiuchumi. 

Pia amewaomba wananchi wenye ulemavu kama yeye na wasio na ulemavu kuacha kubweteka na badala yake wachangamkie fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali katika viwanda na pia wajiajiri badala ya kukaa nyumbani na kukata tamaa.

“Ni waombe  walemavu wenzangu na wasio walemavu kuacha kubweteka wajitume; kama mimi naweza kwanini wewe ushindwe  pia niwakaribishe watu mbalimbali wenye ujuzi hususan walemavu waje katika ofisi yangu tushirikiane kazi ili tujenge uchumi wa taifa letu, najisikia vibaya nikiwaona vijana hawafanyikazi wanaombaomba, ifike wakati tuache kuombaomba,” anasema Singano.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot