![Image result for ZEBAKI](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgAB3t_dVblP0yBPO4y2F2vMjsJ-HmeOyQ13dnSDnJ2BJ38KVR7615dV0iyZUB0pdRUszhdz2fiVjOz7RWR9i_2tSZYInAiQphio1G-fqa3Gr8YQiDMm-lsDw3y5QfFLtsHgMzzPlnFtlg/s640/_69501639_zama_babygirl.jpg)
.Wachimbaji wanena bila
hofu: Eti kwao ni kawaida!
NA JAMES ZAKAYO, MARA
DALILI zinazoashiria
ugonjwa wa saratani zimejitokeza miongoni mwa wachenjuaji wa dhahabu katika
mgodi wa Kebaga, kata ya Kenyamanyori Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara
kutokana na matumizi makubwa ya kemikali aina ya zebaki (mercury).
Lakini
kushangaza baadhi ya wachenjuaji hao hawana hofu na hali hiyo wakisema kuwa ni
sehemu ya maisha yao ingawa wataalamu wanasema ni hatari kwao.
Uchunguzi
umebaini kuwa watu hao hutumia zebaki kuchenjua dhahabu kwa mikono jambo ambalo
limewaathiri baadhi yao kubadilika rangi ya asili ya mwili ikiwa ni dalili
mbaya.
Mwita
Marwa ni mmoja wao, anapozungumza na mwandishi wetu anaonekana mwenye uso wa furaha
katika kile anachokifanya licha ya kuwa haelewi kinachobadili rangi ya asili ya
viganja vya mikono yake kuwa pinki.
“Kubadilika kwa rangi ya mkono huu ni hali ya
kawaida kwani ndio kazi zetu. Miaka yote wazee wetu wamechimba dhahabu na
kuosha kwa kutumia kemikali hii lakini bado wapo,” anasema Marwa alipoulizwa na
mwandishi wetu kuhusu hali hiyo. Hata hivyo anakanusha hali hiyo kusababishwa
na matumizi ya zebaki, akidai hutokana na shughuli za uchimbaji za kila siku.
![Image result for ZEBAKI](https://i.ytimg.com/vi/EeT3bbx6qmk/hqdefault.jpg)
Mchenjuaji
mwingine mwanamke, Motera Nyaseba
anakiri kuwa wamewahi kutahadharishwa hatari ya matumizi ya zebaki ingawa anadai kuwa wanalazimika kuitumia ili kupata
pesa.
“Sisi tunafanya hivi ili kuweza kutimiza haja
za familia zetu kutokana na mzigo mkubwa wa sisi wanawake kuwa waangalizi
wakubwa wa familia. Wengine hapa ni wajane. Pia sisi wanawake hatuna uwezo wa
kuingia kwenye mashimo, hivyo wengi tumejikita hapa,”anasema Nyaseba.
Mganga
Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Dk. Boniventure Bisulu anafafanua kuwa
hali hiyo ni matokeo ya kuondoka kwa mafuta asili kwenye ngozi kutokana na watu
hao kushika kemikali ya zebaki mara kwa mara.
“Kemikali hii inapogusana na ngozi huingia
mwilini kupitia matundu ya vinyweleo, huaribu seli na kisha kutengeneza
saratani ya ngozi” alisema Dk. Bisulu.
Kutokana
na shughuli ya uchenjuaji kufanywa kila
siku, pia madini hayo hupenya mwilini bila mtu kujua na kujikita ndani ya mfumo
wa kutengeneza damu na kwenye mifupa kisha kuzuia utengenezaji wa damu jambo ambalo husababisha upungufu wa damu (anemia).
“Kemikali
hii inapokuwa inaendelea kushambulia sehemu ya kutengenezea damu, baadae hutengeneza ugonjwa wa saratani ya damu
ujulikanao kwa jina la kitalaamu la leukemia,” anasema Dk. Bisulu.
Zaidi,
huharibu mfumo wa fahamu na kusababisha mtu kuwa na tatizo la kupoteza
kumbukumbu mara kwa mara (dementia), kukosa usingizi na misuli kuchoka.
Naye
Dk. Innocent Kweka wa hospitali hapo, anasema zebaki ni moja ya kemikali zilizo
katika kundi lijulikanalo kitalaamu kama in-organic ambapo kundi la kemikali hizo zina madhara
yanayofanana. Pamoja na saratani madhara mengine ni kuharibu mfumo wa fahamu
ambao husababisha ugonjwa wa kutetemeka, kupoteza kumbu kumbu na mengine.
“Hata
hivyo madhara yake hutofautiana kulingana na kiwango kilichoingia mwilini.
Jambo moja kubwa, ifahamike kwamba
zebaki ina tabia ya kushambulia seli
bila kujali kiwango,”anasisitiza Dk. Kweka.
Pia
huweza kusababisha madhara kwa kunywa maji yenye viambata vya kemikali hiyo, ikigusa
ngozi na kwa kuvuta puani ingawa dalili katika mfumo huo wakati mwingine
hutofautiana, alisema.
Mkemia
Rwige Ogunya wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa anakiri madhara
yanayoelezwa na waganga hao na kuongeza kuwa, zebaki hushusha kinga ya mwili.
Ogunya
anasema licha ya wachimbaji, wachenjuaji na jamii kuelimishwa mara kwa mara
kuhusu madhara hayoi, baadhi yao wamekuwa wakaidi.
“Wanatakiwa kufuata njia salama za kukamatia
madini hayo kwa kutumia vifaa vya kuzuia au kupunguza madhara mwilini,”anasema
Ogunya na kutaja vifaa hivyo kuwa ni vile vya kufunika mdomo, pua wakati wa
kuchenjua, kujikinga na moshi wakati wa kuchoma dhahabu ili moshi wa zebaki
usiwapate kwa namna yoyote.
Utafiti
uliofanywa na kuandikwa katika jarida moja (sio Tanzania) liitwalo AMJ
public health uliohusisha wachimbaji wadogo wa dhahabu huko mgodi wa
Rwamagasa Geita hapa nchini ulieleza kuwa shughuli za wachimbaji wadogo wa
madini hayo huongoza kwa matumizi ya zebaki.
Utafiti
huo ulionesha kuwa watu milioni 80 hadi 100 kwenye nchi zinaoendelea ikiwamo
Tanzania hutegemea uchimbaji wa madini. Kati yao, milioni 13 hadi 15 huzalisha tani 500 mpaka
800 za dhahabu duniani kila mwaka.
Ili
kupata tani hizo za dhahabu ni lazima tani 800 hadi 1,000 za zebaki zitumike
jambo ambalo linatajwa kuwa ni chanzo kikubwa cha matatizo ya kiafya.
Naye
Dk. Jonh Astete wa taasisi moja afya y nchini Peru anasema katika utafiti
uliofanywa na taasisi yake ilibainika kuwa waathirika wakubwa wa zebaki ni watu
wanaoishi pembezoni mwa migodi wengi wao wakijishughulisha na uchenjuaji wa
dhahabu.
Utafiti
huo ulihusisha watu 200 wanaozunguka maeneo ya mgodi katika mji wa Huepetuhe
nchini humo na kuonekana kuwa ni rahisi kemikali hiyo kuenea kwa njia ya hewa
na kudhuru maeneo ya jirani.
Taarifa
ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inasema limekuwa katika mapambano dhidi ya
matumizi ya kemikali kwa kuzihamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Matifa
kusimamia marufuku iliyowekwa, ingawa usimamizi wa sheria na marufuku hiyo ni
kikwazo hasa katika nchi zinazoendelea.
Tanzania
kupitia kamati ya Kitaifa ya Kimkakati (NAP) chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais
ilitia saini mkataba wa Minamata nchini Japan
unaolenga kupunguza na kuondoa matumizi ya kemikali ya zebaki licha ya
kemikali hiyo kuendelea kuwepo
hapa nchini.
Taarifa
ya wizara ya Nishati na Madini (sasa Madini) inasema kuwa Serikali
imetambulisha kemikali ya Borax kwa uchenjuaji wa dhahabu kama mbadala wa
zebaki ingawa baadhi ya wachenjuaji
wamekuwa wakidai kemikali hiyo haiwasaidii,
kuendelea kutumia ile hatarishi.
Kwa
mujibu wa Taarifa hiyo, serikali imekusudia kutengeneza vituo maalumu vya
kisasa ili kufundishia wachimbaji wadogo njia bora za uchenjuaji wa madini hayo
bila madhara.
Ikumbukwe
kuwa tukio kama hilo katika mgodi wa Kebaga liliwahi kutokea mwaka 2009 katika
mgodi wa North mara uliopo Tarime kumwaga maji yenye kemikali katika mto Tigite
na kusababisha athari za kiafya kwa binadamu na mifugo, ambapo watu kadhaa
walipoteza maisha.
Mgodi
wa Kebaga unategemewa na watu kutoka vijiji vya kata ya Kenyamanyori yenye watu 11,000
. Pia hutegemewa na baadhi ya wanavijiji
wa kata ya Turwa.
Baadhi
ya dalili za mtu aliyeathiriwa na zebaki ni pamoja na ngozi ya mikono kuwa kavu
na kubadilika rangi kuwa nyekundu, nyeusi ama pinki.
Zingine
ni mwili kudhoofu, kukosa hamu ya kula, uoni hafifu, kupungua uzito, maumivu ya
tumbo, kichefuchefu, kuvimba fizi na vidonda mdomoni.
![Image result for ZEBAKI](https://i.ytimg.com/vi/EeT3bbx6qmk/hqdefault.jpg)
No comments:
Post a Comment