Mwanafunzi wa Shule ya Uandishi wa Habari na
Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Steven Mkomwa
akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati alipokuwa akizindua
makala yake ya ‘habari na mtoto’ kuelekea katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto
Duniani yanayofanyika Novemba 20 ya kila mwaka. Mkutano huo umefanyika leo
Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO.
NA RASHID HASSAN,
SERIKALI
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetakiwa kutoa motisha
na kutoa tuzo maalum kwa waandishi wa habari wanaoandika habari, makala
na kuandaa vipindi vya kuelimisha jamii kuhusu haki na utetezi wa watoto.
Wito
huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mwanafunzi wa Shule ya Uandishi wa
Habari na Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Steven Mkomwa wakati alipokuwa akizindua makala yake ya ‘habari na mtoto’ kuelekea
katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani yanayofanyika Novemba 20 ya kila
mwaka.
Mkomwa alisema kuwa ufinyu wa ushirikiano kati ya
vyombo vya habari na Asasi za Kiraia au Wizara yenye dhamana ya watoto ni moja
ya kikwazo katika suala zima la utetezi wa mtoto hivyo ni vyema kuboresha na
kuyadumisha maudhui haswa pale wadau wanapoonesha utayari wao katika kupigania
ustawi wa watoto nchini.
“Sisi
kama Taifa kupitia Wizara yenye dhamana ya watoto iko haja ya kutambua michango
ya wanahabari wanaokwenda maili za ziada katika kuripoti na kumtetea mtoto kwa
kutoa tuzo za motisha na utambuzi ili kutengeneza na kuchochea mazingira ya
habari za kina na zenye uhalisia”, alisema Mkomwa.
Mkomwa
ameongeza kuwa ili kuchochea mchakato wa utoaji wa tuzo hizo, amedhamiria
kuandika barua ya wazi kwa Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya watoto kwa
kujenga hoja na kushawishi ni kwa namna gani mchakato huo unavyoweza kufanyika
kwa kushirikisha wadau wa haki za watoto na huduma kwa watoto.
Akifafanua
zaidi, Mkomwa alisema kuwa kuwa tuzo hizo zinaweza kufanyika kila mwaka kwa
kutambua michango ya vyombo vya habari kupitia waandishi wa habari wenye
jitihada za kuandika habari za kutetea watoto, wahariri, wamiliki au wasimamizi
wa vyombo husika vya habari pamoja na wadau wengine nje ya tasnia ya habari.
Aidha
aliiomba wizara hiyo pamoja na wananchi kujifunza kutokana na matokeo
yaliyotolewa katika utafiti uliofanywa na shirika la Internews Europe mnamo
mwaka 2013 ambao uligundua kuwa kuna ufinyu wa sauti za watoto katika mikondo
ya Vyombo Vikuu vya Habari kuandaaa viwango, taratibu na miongozo ya kitaaluma
katika kuripoti habari dhidi ya haki kwa mtoto.
Tarehe
20 Novemba ya kila mwaka, Dunia inaadhimisha Siku ya Mtoto Duniani ambayo ni
mahsusi katika kuonesha umuhimu wa ulinzi na utetezi kwa mtoto pamoja na
kufanya tathmini za kikanda na kidunia juu ya viwango vya ukiukwaji na ukatili
wa haki za watoto.

No comments:
Post a Comment