![]() |
| Waziri wa Madini nchini Tanzania Angellah Kairuki |
WAZIRI wa Madini Angellah Kairuki mwishoni mwa wiki
alikutana na Ujumbe wa Benki ya Dunia jijini Dar es Salaam kwa lengo la
kufahamiana na kuangalia hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa
Miradi ya Madini inayotekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa
Rasilimali Madini (SMMRP) unaofadhiliwa na Benki hiyo kwa kushirikiana na
Serikali.
Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa katika
kikao hicho, Waziri Kairuki aliitaka Benki ya Dunia kuona namna ya kuwaendeleza
Wataalam wa Sekta ya Madini ili kuwezesha uwepo wa Watalaam wa kutosha hususan
katika masuala ya Uthaminishaji wa Madini ya Almasi, Tanzanite na madini
mengine ya vito na pia masuala ya uongezaji thamani madini kwa ujumla.
Pia, alishauri
umuhimu wa kuboreshwa kwa Mtandao wa Huduma za Leseni kwa Njia ya Mtandao
(Online Mining Cadastre) ikiwa ni pamoja na kuunganisha mtandao huo na Mamlaka
nyingine ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa
Jiolojia Tanzania (GST) ili taarifa zote zinazohusu madini na mapato yatokanayo
na madini ziweze kupatikana kupitia mtandao huo.
Vilevile, aliishauri Benki hiyo kuhusu
uuzwaji wa Madini ya Almas kwa njia ya Mnada kama vile inavyofanyika kwa Madini
ya Tanzanite, lengo likiwa ni kuwezesha Serikali kunufaika na madini hayo.
Aliongeza kuwa, baada ya Serikali ya Tanzania
kupitisha Marekebisho ya Sheria ya Madini kupitia Sheria ijulikanayo kama (The
written laws (Miscellaneous Amendements) Act, 2017), alisema kuwa, baadhi ya
wawekezaji wameonesha wasiwasi kuhusu marekebisho hayo.
Hivyo, Waziri Kairuki amewataka wawekezaji
kutokuwa na hofu kwani mabadiliko hayo yanalenga kuhakikisha kuwa Serikali
inanufaika ipasavyo kutokana na rasilimali zake za madini. Aidha, alisema
kwamba, nia ya Serikali kuhusu kuvutia wawekezaji iko palepale ilimradi
wazingatie Sheria na taratibu.
Vilevile Waziri Kairuki alieleza kwamba, ni
vema Benki ya Dunia ikaangalia namna bora ya kuhakikisha madini yote ya
Tanzanite yanayouzwa nje ya nchi yanakuwa na Hati ya Uhalisia inayoonyesha
chanzo cha madini hayo suala ambalo litawezesha Taifa kupata mapato stahiki kutokana
na rasilimali hiyo.
Vievile, Waziri Kairuki alizungumzia suala la
udhibiti wa utoroshaji madini na kusisitiza kuhusu kuwepo na namna bora ya
kuzuia utoroshwaji wa madini ya Tanzanite ikiwemo kujulikana kwa idadi ya
wachimbaji wadogo, wa kati, kiasi kinachopatikana na mahali madini hayo
yanapouzwa.
Pia, Waziri Kairuki aliishukuru Benki ya
Dunia kutokana na ushirikiano ambao umekuwepo baina ya Serikali kwa kipindi
chote na kueleza kuwa, Serikali iko tayari kutekeleza miradi husika kikamilifu
kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa
Simon Msanjila aliiomba Benki ya Dunia kuleta Wataalam wa madini nchini
ili waweze kutoa mafunzo katika vituo vya Madini nchini ikiwemo Chuo cha Madini
Dodoma (MRI) na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ili kuzalisha wataalam zaidi
katika Sekta hiyo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Tanzania
Mhandisi Benjamin Mchwampaka alisema kuwa, tayari Serikali imefanya jitihada
kadhaa za kuanzisha mfumo wa utoaji wa leseni kwa njia ya Mtandao. Aliongeza
kuwa, kinachotakiwa sasa ni kuimarisha zaidi mfumo huo ili taarifa zote
zinazohitajika na umma zinazohusu madini na mapato ya kodi na mrabaha ziweze
kupatikana kwa urahisi na kwa uhakika.
Aidha, Kamishna Mchwampaka aliiomba Benki ya
Dunia kukijengea uwezo zaidi Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kilichopo
jijini Arusha ili kiweze kutoa mafunzo ya Utambuzi wa madini na Uongezaji
thamani kwa viwango vya Kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya
Dunia Bella Bird alisema zipo fursa nyingi kwa Sekta ya madini na hivyo kuiomba
Wizara ya Madini kuhakikisha kuwa inatumia fedha zilizopo katika miradi husika
na kwa wakati.
Naye, Mwakilishi Mwandamizi Mradi kutoka
Benki ya Dunia ambaye pia ni Mtaalamu wa Madini kutoka Idara ya Nishati
Endelevu nchini Merekani, Mamadou Barry, alisema kuwa, Wizara ya Madini
ihakikishe kuwa inakamilisha ujenzi wa Kituo cha Madini kinachotarajiwa
kujengwa eneo la Mererani kwa wakati ili kuwezesha minada ya
madini na maonesho ya madini kufanyika kwenye kituo hicho, na hivyo kudhibiti
utoroshwaji wa madini.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Masula ya Madini
kutoka benki hiyo Sheila Khama aliishauri Serikali ya Tanzania kuona namna ya
kushirikiana na nchi nyingine kama Afrika Kusini hususan kwenye Mikutano ya
Uwekezaji madini ya Indaba ili kuendelea kuwavutia wawekezaji.
Aidha, alishauri Tanzania kujifunza kutoka
nchi ya Ethiopia kuhusu namna ya kudhibiti Wachimbaji Wadogo wa madini ya
dhahabu kwa kuwa, nchi hiyo unao mfumo bora Barani Afrika.
Pia, alisisitiza kuhusu umuhimu wa
ushirikishwaji wa wanawake katika shughuli za madini nchini.

No comments:
Post a Comment