NA MWANDISHI WETU.
KIUNGO wa Simba SC, Said Hamisi Ndemla sasa ataondoka
nchini Alhamisi kwenda Sweden kufanya majaribio katika klabu ya AFC Eskilstuna badala ya leo kama ilivyoelezwa awali.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu ya Simba, Hajji Sunday Manara amesema leo katika taarifa yake kwa vyombo vya
Habari kwamba, mabadiliko hayo hayataathiri muda wake wa majaribio katika klabu
hiyo, ambao ni siku
14.
|
Said Ndemla mwenye jenzi nyekundu(14) wa Klabu ya Simba pichani.
Aidha Jana Manara alisema; “Klabu inaamini Ndemla
atafanya vizuri na kufuzu katikamajaribio hayo .Kama itakuwa tofauti na hivyo,
mchezaji huyo ataendelea kuichezea Simba. Huu ni utaratibu wa klabu wa kuwapa
nafasi wachezaji wake kwenda nje kujaribu bahati zao za kucheza soka la kulipwa,”.
Akifanikiwa kufuzu majaribio katika klabu hiyo,
Ndemla mwenye umri wa miaka 21 ataungana na Mtanzania mwingine, mshambuliaji
Thomas Ulimwengu, ambaye kwa sasa ni majeruhi anasumbuliwa na maumivu ya goti
tangu Septemba, mwaka huu na atakuwa nje hadi Januari mwakani.
Ndemla aliibukia kikosi cha timu ya vijana ya Simba, maarufu kama Simba B mwaka
2012 kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa mwaka 2013 na tangu mwaka 2015
amekuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka
Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu
katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010
alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011
alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
Alicheza U-20 ya Mazembe msimu moja
kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi
anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
Aidha Ulimwengu amehamia Ulaya baada ya kushinda
mataji makubwa akiwa na Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup
ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.
|
No comments:
Post a Comment