WAZIRI
wa Maliasili na Utalii nchini ,Dk.
Hamisi Kigwangalla amesema Serikali kupitia Wizara yake inakusudia kuandaa
mkakati maalum wa kutangaza vivutio vya utalii
Tanzania nchini China ili kuongeza idadi ya watalii na mapato
ya Serikali.
Aidha Dk. Kigwangalla
amesema hayo jana ofisini kwake mjini Dodoma akiwa kwenye mazungumzo na Balozi
wa China nchini, Mhe. Wang Ke ambaye alimtembelea kwa ajili ya kujitambulisha na
kujadili mambo mbalimbali ya kuimalisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili
katika sekta ya Uhifadhi na Utalii.
“Moja ya mkakati wangu
kama Waziri mpya wa Wizara hii kukuza utalii ni kuweka mkakati wa kuleta
watalii wengi kutoka China, China ni Taifa Kubwa lenye watu wengi, tunalenga
zaidi kuwafikia watu wanaoishi maisha ya kati ambao ndio wanaopenda kutumia
fedha zao kufurahia maisha” Alisema Dk. Kigwangalla
Ambapo katika
mazungumzo hayo alimuomba Balozi huyo kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa njia ya ushauri wa kitaalamu au wa kifedha
kwa ajili ya kuandaa mkakati mahususi wa kulifikia soko la utalii la China kwa
kuainisha vivutio na aina ya
huduma ikiwemo hoteli ambazo zitakuwa kivutio kwa
watalii kutoka China kuweza kutembelea Tanzania.
Miongoni mwa mikakati
waliojadiliana ni uwezekano wa kutumia fursa ya uwepo wa wawakilishi wa
Televisheni ya CCTV ya China nchini Tanzania ambao wanaweza kutumika kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini
ikiwemo kuambatana na Waziri Kigwangalla
kwenye ziara zake za kikazi kwenye
maeneo ya vivutio na baadaye kuvitangaza nchini China na Duniani kote.
Hata hivyo walijadili
pia uwezekano wa kuanzisha safari za moja kwa moja za ndege baina ya nchi hizo
mbili kwa lengo la kurahisisha Safari za Utalii pamoja na kuanzisha mtandao wa
pamoja wa watoa huduma za utalii wa mataifa hayo mawili.
Aidha, Dk. Kigwangalla
alimuomba balozi huyo kuleta wawekezaji katika sekta ya Hoteli za kitalii na
kuahidi kuwapa maeneo ya kujenga hoteli hizo ili kukuza huduma na soko la
utalii nchini kwa kurahisisha upatikanaji wa watalii wa China kutembelea
Tanzania.
Kwa upande wake Balozi
Wang Ke alimueleza Waziri Kigwangalla kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na
Tanzania katika nyanja mbalimbali ambapo mwezi Februari mwakani (2018) itaandaa
Maonyesho ya Kimataifa ya Kuuza Nje na Kuingiza Bidhaa na Huduma (International
Export and Import Fair) ambapo watu mashuhuri kutoka China watashiriki akiwemo
mcheza Filamu mashuhuri kwenye filamu ya kichina kwa Lugha ya Kiswahili
maarufu kama Maododo.
Alisema kupitia
Maonyesho hayo Tanzania itaweza kujenga mtandao wa utalii na China kwa kunadi
vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini kwa watu maarufu watakaoshiriki
maonyesho hayo wakiwemo wafanyabiashara na watoa huduma za utalii na ukarimu.
No comments:
Post a Comment