NA MWANDISHI WETU.
MSTAHIKI Meya wa jiji la Dar
es Salaam Isaya Mwita amefungua ukurasa mpya wa uhusiano wa miji dada kwa
kusaini mkataba mpya kati ya jiji la Hamburg na Dar es Salaam.
Mkataba huo umesainiwa Novemba
14, mwaka huu katika Jiji la Hamburg ambapo Meya Mwita na Mstahiki
Meya wa Jiji la Hamburg, Olaf Scholz, walisaini mkataba huo na
kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana.
Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita kushoto akisaini mkataba wa kurudisha uhusiano na jiji la Hamburg.kulia ni Meya wa jiji la Hamburg. |
Wengine walioshuhudia tukio
hilo ni , watendaji wakuu wa mamlaka ya Jiji la Hamburg na Taasisi mbalimbali
za Serikali katika Jiji hilo, wawakilishi wa asasi za kiraia na baadhi ya
Watanzania wanaoishi jijini Hamburg.
Mkataba wa awali wa uhusiano
huo ulitiwa saini mwaka 2010 na Adam Kimbisa na Ole Van
Beust waliokuwa mameya wa majiji hayo katika kipindi hicho.
Mstahiki Meya na Mkurugenzi
wa Jiji la Dar es Salaam waliwasili katika Jiji la Hamburg kwa ziara ya kikazi
na kusaini mkataba huo wakitokea katika mji wa Bonn ambako walishiriki katika
mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi ulioandaliwa na taasisi ya Engagement
Global ya Ujerumani kwa miji washirika wa Ujerumani.
Viongozi hao wawili wa
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakiwa mjini Bonn walishiriki pia katika
mkutano wa mameya na magavana ambao ulikuwa sehemu ya mkutano ulioandaliwa na
Umoja wa Mataifa wa COP 23 ambao umefanyika sambamba na mkutano ulioandaliwa na
Engagement Global.
Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita akisaini mkataba wa kurudisha uhusiano na jiji la Hamburg. |
Kabla ya kusainiwa kwa
mkataba huo, vikao vya wataalam mbalimbali wa Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam, Engagement Global, miji wa shirika na wataalam wa Wizara ya Maendeleo
ya Miji na Makazi wa Jiji la Hamburg, vilifanyika mjini Bonn na Hamburg kwa
usimamizi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa
Jiji la Hamburg, Wolfgang Schmidtz,.
Aidha katika mkutano
huo walibaini maeneo mengi zaidi ya ushirikiano kati ya miji hiyo,
wahusika na miradi mipya inayoweza kutekelezwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya
wananchi kupitia uhusiano huo.
Pande hizo mbili, hasa kwa
kuzingatia matwaka ya Dar es Salaam, zimekubaliana kushirikiana katika maeneo
ya mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma
kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo, upangaji wa miji, uboreshaji wa
huduma za usafiri wa umma na shughuli za kukuza utalii katika Jiji la Dar es
Salaam.
Hata hivyo baada ya kusainiwa
kwa mkataba huo, viongozi hao wa Jiji la Dar es Salaam walikutana na Bodi ya
Ushauri ya Jiji la Hamburg na kisha kuwa na mkutano mwingine na wadau wa
uhusiano huo wakiwemo Watanzania wanaoishi Hamburg ambao wajumbe wote kwa
ujumla walisisitiza kila upande ufanye jitihada za dhati za kuimarisha
ushirikiano huo kwa kuacha urasimu.
Hii ni safari ya kwanza ya
kikazi nje ya nchi kwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mwita na
Mkurugenzi wa Jiji hilo, Sipora Liana, kusafiri pamoja na kurejea nchini wakiwa
wamefanikiwa katika kutimiza malengo ya safari yao mjini Bonn na Hamburg
No comments:
Post a Comment