NA MWANDISHI WETU, MWANZA
MFANYABIASHARA mmoja ambaye
ni mzaliwa wa wilayani Kwimba mkoani Mwanza, ametoa msaada wa vitu mbalimbali
wenye zaidi ya shilingi milioni 27, kwenye sekta ya afya na elimu katika wilaya
hiyo, kama fadhira yake akiwa mmoja wa wazawa wa wilaya hiyo.
Mwananchi huyo Richard
Mchele, alitoa msaada huo juzi ambao ni pamoja na madawati katika shule tatu za
msingi, ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika shule mbili za msingi,
ujenzi wa vyoo viwili vyenye matundu manane ya wasichana na wavulana, pamoja na
mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya.
Wakipokea msaada huo
kwa nyakati na maeneo tofauti, wananchi, walimu, viongozi pamoja na wanafunzi
walimshukuru mwananchi huyo kwa kukumbuka kwao na kuamua kutoa
msaada huo.
Sostenes Shibula ni
mwenyekiti wa kati ya shule ya msingi Nyashana, pamoja na Vicent Mulesa ambaye
ni mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo ni kati ya wananchi waliotoa shukuruani
zao kwa mwananchi huyo.
Walisema kuwa afya za
wanafunzi zilikuwa hatarini kwa sababu ya shule hiyo kukosa vyoo na kwamba
nusura ifungwe kwa sababu ya changamoto hiyo.
“Msaada aliotupatia
huyu ndugu yetu tumeupokea kwa mikono miwili, maana afya za watoto wetu
zilikuwa mashakani maana hakukuwa na choo na serikali ilikuwa inataka kuifunga”
alisema Sostenes Shibula.
Akikabidhi msaada huo
Richard Mchele, alisema kuwa lengo lake ni kusaidia kule alikotoka, huku
akiitaka jamii kushirikiana naye katika kuboresha elimu na kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Joseph Pombe
Magufuli katika masuala mbalimbali, ikiwemo sekta ya elimu.
Mchele alisema kuwa
aliamua kutoa msaada huo nyumbani kwao kwa sababu ndiko alikozaliwa na kwamba
pia hatua hiyo nikuunga mkono juhudi za rais Magufuli katika kuletea wananchi
maendeleo.
“Huku ndiko kwetu
hivyo nimeamua kutoa msaada huu, ambao wote umegharimu zaidi ya shilingi
milioni 27, nikiunga mkono juhudi za rais wetu katika suala zima la kuletea
wananchi maendeleo hususan katika sekta ya afya na elimu” alisema.
Mmoja wa wenyeviti wa
vijiji ambavyo vimefaidika na msaada huo, Mahenge Joseph, alisema kuwa msaada
huo ni mkombozi kwao na kuomba wananchi wengine wenye kipato kuiga mfano wa
mfanyabiashara huyo.
Mfanyabiashara huyo
pamoja na wenzake wamekuwa na tabia ya kutoa misaada ya kijamii katika mikoa ya
kanda ya ziwa, kama fadhira yao kwa kukumbuka kule waliokozaliwa.
No comments:
Post a Comment