PALESTINA,
Imeandikwa na Rais wa Taifa la Palestina,Mheshimiwa Mahmuud Abbas
Waingereza wengi hawamjui
“Sir.Arthur James Balfour”ambae aliwahi kuwa Waziri Mkuu mwanzoni mwa
karne ya ishirini, lakini jina lake ni maarufu sana kwa Wapalestina
wapatao milioni kumi na mbili. Katika kumbukumbu ya azimio la
Balfour,serikali ya Uingereza inalazimika kutumia fursa hiyo ili
kurekebisha makosa ya kihistoria iliyoyafanya dhidi ya wananchi wetu wa
Palestina.
Mnamo Novemba 2,1917 akiwa ofisini
kwake mjini London,“Sir.Arthur James Balfour”alisaini barua akiliahidi
shirika la kizayuni, kuanzisha taifa lao ndani ya ardhi ya Palestina.
Ameahidi kutoa ardhi hiyo wakati sio yake, huku akifumbia macho haki za
kisiasa za Wapalestina walioishi katika ardhi hiyo kwa miaka mingi. Kwa
Wapalestina ambao ni raia wangu, matukio yaliyosababishwa na barua hii
yamekuwa na uharibifu mkubwa, huku pia yakiacha madhara ya muda mrefu
kwa wananchi wetu.
Sera ya Uingereza iliyounga mkono
uhamaji wa Wayahudi kwenda Palestina, ikiwa ni mbadala wa kukataa kwao
haki ya Kiarabu ya Palestina ya kujipangia mustakabali wao, sera hiyo
imeleta mvutano mkali kati ya wahamiaji wa Kiyahudi wa Ulaya na wakazi
wa asili wa Kipalestina. Palestina iliyokuwa ajenda ya mwisho ya
kumaliza ukoloni, inasumbuka kama tunavyosumbuka wananchi wake kutafuta
haki yetu isiyo badilika katika kujipangia mustakabali, jambo ambalo ni
janga kubwa mno kushuhudiwa na historia ya sasa.
Rais wa Taifa la Palestina,Mheshimiwa Mahmuud Abbas |
Mnamo mwaka 1948, wanajeshi wa
kizayuni waliwafukuza kwa mabavu kutoka katika miji yao, watu wanaofikia
milioni moja wakiwemo wanawake na watoto, huku wakifanya mauaji ya
kutisha na kubomoa kabisa vijiji kadhaa. Wakati tulipofukuzwa kwa mabavu
kutoka mji wa Safad, umri wangu ulikuwa miaka kumi na tatu, wakati
Israel ikisherehekea kuasisi taifa lake, sisi Wapalestina tunakumbuka
siku ya giza zaidi katika historia yetu.
Azimio la “Balfour” kwa hakika sio
tukio la kusahaulika, kwani wananchi wangu leo wanaofikia zaidi ya
milioni kumi na mbili wamesambaa duniani kote, baadhi yao wakilazimishwa
kwa nguvu kuacha miji yao mnamo mwaka 1948, huku zaidi ya Wapalestina
milioni sita bado wanaishi uhamishoni hadi leo hii, waliosalia katika
miji yao ni milioni (1.75) ila wao wanaishi chini ya mfumo wa kibaguzi
uliopangika nchini Israel.
Aidha, Wapalestina zaidi ya
milioni (2.9) wanaishi Ukingo wa Magharibi wakiwa chini ya uvamizi wa
kijeshi na wa kinyama uliogeuka kuwa ni ukoloni. Miongoni mwao wapo
wakazi wa Jerusalem ambao ni wa asili kabisa wapatao laki tatu
(300,000), bado wanapambana na sera za kivamizi za Israel
zinazowahamisha kwa nguvu kutoka katika mji wao. Huku wapalestina
wengine wapatao milioni mbili wapo katika Ukanda wa Gaza, ambayo ni
gereza la wazi linaloharibiwa mara kwa mara na vifaa vya jeshi la
Israel.
Azimio la “Balfour” kwa hakika
sio mnasaba wa kusherehekea, hasa katika wakati ambao bado upande mmoja
unadhulumiwa na unapata dhiki kwa sababu ya azimio hilo, kuasisiwa kwa
taifa la watu fulani, kumepelekea kufukuzwa kwa watu wengine na
kuendelea kukandamizwa, haiwezekani kulinganisha kati ya mvamizi na
taifa linalokaliwa kimabavu. Ni lazima kulisawazisha kosa hili ambalo
Uingereza inabeba jukumu kubwa na inalazimu sherehe hizo zifanywe katika
siku ambayo, wakazi wote wa ardhi hii wakiwa katika uhuru, heshima na
usawa.
Tukio la kusaini azimio la
“Balfour”, limeshatokea na halibadiliki lakini ni jambo ambalo yapasa
kurekebishwa, jambo hili linahitaji unyenyekevu, ushujaa, kukubali
yaliyopita, kukiri makosa na kuchukuwa hatua stahiki za kurekebisha
makosa hayo. Nami katika mtiririko huu, ninapongeza ushujaa wa wananchi
wa Uingereza wanaoitaka serikali yao kuchukua hatua kama hizi zifuatazo:
Wabunge 274 wamepiga kura ya kulitambua taifa la Palestina, wakati
maelfu ya wananchi wakiitaka serikali yao kuomba radhi kwa azimio la
Balfour, huku makundi kadhaa na asasi za kiraia zikiandamana kuunga
mkono haki za taifa letu bila usumbufu wowote.
Pamoja na mateso tuliyokumbana
nayo karne iliyopita, bado wananchi wa Palestina wamesimama kidete,
kwani sisi ni wananchi tunaojifaharisha kwa urithi wake mwingi,
ustaarabu wake mkongwe na kwa kutambua ya kwamba Palestina ndio chimbuko
la dini tatu za mbinguni. Ukweli wa mambo, tumezoea kwa miaka mingi
kuishi na matukio yaliyotuzunguka, ambayo yamesababishwa na mtiririko wa
matukio yaliyoanza mwaka 1917, tukafikia makubaliano machungu kwa ajili
ya kufikia amani, kuanzia kukubali kuasisiwa taifa la Palestina kwa
asilimia 22% tu ya ardhi ya kihistoria, kulitambua taifa la Israel bila
ya sisi kutambuliwa hadi leo hii.
Tukawa na msimamo wa ufumbuzi wa
dola mbili kwa muda wa miaka thelathini iliyopita, msimamo ambao
utekelezaji wake umekuwa hauwezekani pamoja na muda kupita. Hivyo basi,
muda wa kuwa Israel inaendelea kupata kinga na misaada kutoka jamii za
kimataifa, badala ya kuichukulia hatua kwa ukiukaji wake unaoendelea
dhidi ya misingi ya sheria za kimataifa, jambo hilo halitaihamasisha
kuacha uvamizi wake na lazima huu utakuwa ni mtazamo dhaifu.
Inapasa kwa Israel na marafiki
zake kutambua vizuri kuwa, ufumbuzi wa kuwepo dola mbili unaweza kwisha
kabisa, isipokuwa taifa la Palestina litabaki hapa na kuendelea na
juhudi zake ili kurudisha uhuru wake, iwe kupitia ufumbuzi wa dola mbili
au mapambano kwa ajili ya kujipatia haki sawa kwa kila mkazi wa
Palestina ya kihistoria.
Muda umefika sasa kwa serikali ya
Uingereza kuchukua nafasi yake, kwani kuchukua hatua stahiki kunalenga
kumaliza uvamizi kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio yake,
likiwemo azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama namba 2334 na
kulitambua taifa la Palestina kwa mujibu wa mipaka ya mwaka 1967, lenye
mji mkuu wake Jerusalem ya Mashariki. Kufanya hivyo, kutapeleka mbele
upatikanaji wa haki za kisiasa za wananchi wa Palestina, kuondoa dhulma
kwa wananchi hao na usawa wa haki zake za kisheria, bila shaka
utachangia kupatikana amani iliyo sawa ya uadilifu na ya kudumu katika
Mashariki ya Kati kwa Wapalestina, waisrael na mataifa mengine ya eneo
husika.
Mahmoud Abbas, Rais wa taifa la Palestina na Mwenyekiti wa Kamati ya utendaji ya P.L.O.
No comments:
Post a Comment