NA
MWANDISHI WETU.
MVUA za vuli zilizoanza wiki zimesababisha madhara makubwa
katika mikoa mbalimbali ikiwamo ya Pwani na Dar es Salaam kiasi cha barabara
kufungwa, mabasi yaendayo haraka kusimamisha huduma kwa muda, watu wawili kufa
na saba kunusurika kusombwa na maji.
Aidha, kwa mara ya kwanza Kituo cha
kupimia mvua cha Kibaha mkoani Pwani kimetumia saa 24 kupima milimita 177.9 za
mvua tangu kilipoanzishwa mwaka 1964, upimaji huo umeanzia juzi saa tatu
asubuhi mpaka jana muda huo, hivyo kuweka rekodi.
Jijini Dar es Salaam, kutokana na
mvua zilizonyesha katika maeneo mbalimbali kwa siku mbili mfululizo, Jeshi la
Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kimefunga kwa muda baadhi ya barabara ili
kuzuia maafa zaidi yasitokee.
Kutokana na mvua hizo, vijana wawili
wanadaiwa kupoteza maisha katika maeneo ya Tabata Kimanga na Mbezi Luis
kutokana na kusombwa na mafuriko. Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama
Barabarani, Fortunatus Musilimu alitaja maeneo yaliyofungwa kwa muda kuwa ni Barabara
ya Morogoro eneo la Jangwani, Kibaha Mizani na Barabara ya Mwai Kibaki karibu
na Daraja la Malecela.
“Barabara ya Morogoro kutoka Faya
kwenda Magomeni imefungwa, pia barabara ya Jangwani Klabu ya Yanga kwenda
Kigogo haipitiki na imefungwa...Pia nyumba za kando ya Bonde la Msimbazi
zimefunikwa na maji,” alisema Kamanda Musilimu.
Alisema barabara nyingine
zilizofungwa ni barabara ya Kawawa (Kigogo Sambusa), Kiluvya kwa Komba,
Barabara ya Afrikana karibu na nyumbani kwa Jenerali mstaafu David Mwamunyange,
ambako kuna daraja linalojengwa pamoja na barabara ya Bagamoyo eneo la Tegeta
Nyaishozi mpaka Basihaya.
Aidha, kutokana na hilo, wananchi
wanaotokea Morogoro kwenda Chalinze hadi Dar es Salaam, walishauriwa kutumia
Barabara ya Bagamoyo, wanaotumia Barabara ya Mwai Kibaki watumie Barabara ya
Coca-Cola kwenda Mwenge.
Aidha, Jeshi hilo lilielekeza askari
wa kikosi hicho kwenda katika maeneo ambayo maji yanapita juu ya barabara ili
kuzuia vyombo vya usafiri kutumia barabara hizo. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema wamepata taarifa ya vifo viwili
katika maeneo ya Tabata Kimanga na Mbezi Luis.
“Hadi sasa tuna taarifa ya vifo
Tabata Kimanga katika Bonde la Mto Kenge ambapo kijana anayekadiriwa kuwa na
umri kati ya miaka 25-30 amepoteza maisha na hajatambuliwa na kijana mwingine
ametumbukia na gari yake Mbezi Luis na hajatambuliwa,” alieleza Kamanda
Mambosasa.
Alisema wanaendelea kufanya
ufuatiliaji na tathmini zaidi ya maafa yaliyotokea kutokana na mvua hizo na
watatoa taarifa kamili kwa wananchi. Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa
kampuni ya inayotoa huduma kwenye mradi wa mabasi yaendayo haraka (UDART), Deus
Bugaywa alisema huduma hiyo ililazimika kusitishwa kwa muda jana kutokana na
kufungwa kwa Barabara ya Morogoro kwa sababu ya Daraja la Mto Msimbazi kujaa
maji.
Hata hivyo, huduma ya mabasi
yaendayo haraka iliendelea kutolewa kwa njia ya kutokea kituo cha Gerezani,
Kariakoo kwenda Muhimbili. Kaimu Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa wa Mamlaka ya Hewa Tanzania (TMA), Dk
Ladislaus Chang'a aliliambia gazeti hili kuwa mvua hizo kwa Kibaha ni za
kiwango cha juu kurekodiwa tangu kituo hicho kilipoanzishwa.
“Tokea kituo hiki kilipoanzishwa,
ndani ya saa 24 hatujawahi kupima mvua kubwa kiasi hicho. Mabadiliko ya
tabianchi ulimwenguni viashiria vyake ni matukio ya mvua kubwa," alisema
Dk Chang’a na kuongeza kuwa siku hiyo hiyo vipimo vilionesha kiwango cha mvua
Pemba ilikuwa milimita 42.3, Zanzibar milimita 190.1 na Dar es Salaam milimita
153.3. Alisema katika utabiri wa kila siku unaotolewa na TMA, walitoa angalizo
la uwezekano wa ongezeko la mvua maeneo ya Pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu
Kaskazini Mashariki.
“Hicho ndicho kilichotokea.
Tunatarajia kuanzia leo (jana) mvua itaanza kupungua kidogo katika hayo
maeneo,” alibainisha. Alisema ni vema jamii ikawa na tabia za kufuatilia
taarifa ya hali ya hewa zinazotolewa na kuzingatia kupanga mipango ya kijamii
na kiuchumi, kuweza kuongeza tija na ufanisi pia kuchukua tahadhari kubwa ya
kuokoa mali na maisha.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa
TMA, Dk Agnes Kijazi alipotoa mwelekeo wa mvua za msimu, alisema mvua
zinatarajia kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi nchini.
Alisema matukio ya vipindi vifupi
vya mvua kubwa yanatarajiwa kusababisha mafuriko katika maeneo machache. Mkoani
Pwani, watu saba wamenusurika kifo baada ya kusombwa na maji walipokuwa
wakijaribu kuvuka huku wakiwa wameshikana mikono, ambao walijinusuru kwa
kupanda kwenye miti kabla ya kuokolewa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Aidha, kati ya watu hao, mmoja
alikuwa akining’inia kwa kujishika kwenye bomba la bango la matangazo huku
mwili wake ukiwa ndani ya maji kwa zaidi ya saa huku akiwa anaomba msaada wa
kuokolewa bila mafanikio.
Watu walionusurika ni Kenned
Meshaki, Mohamed Kitindi, Mohamed Zimanya, Furaha Mwaipopo, Silas Moshi, Henry
Francis na mwanamke mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja
ambao wote walikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Pwani ya Tumbi mjini
Kibaha.
Tukio hilo lilitokea jana eneo la
Maili Moja kwenye daraja linalotenganisha kati ya Mkoa wa Dar es Salaam na
Pwani na kusababisha daraja kujaa maji na kusababisha magari na watu kushindwa
kuvuka upande wa pili.
Daraja hilo ambalo linapita kwenye
Mto Mpiji lilikuwa halipitiki na kusababisha watu na abiria kushindwa kuvuka
upande wa pili kutoka Maili Moja wilayani Kibaha na upande mwingine Kiluvya
katika Wilaya ya Ubungo.
Kutokana na daraja hilo kushindwa
kupitika, abiria wa mabasi walishindwa kuendelea na safari zao kupitia kwenye
barabara ya Morogoro. Akizungumza na gazeti hili kwenye eneo la tukio hilo,
Ofisa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Uokoaji, Harrison Mkonyi alisema kazi ya
uokoaji imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani wamewaokoa watu hao wakiwa salama.
“Tunawashukuru wadau mbalimbali
vikiwemo vikosi vya majeshi ya Polisi, Magereza, JWTZ na wananchi ambao
walionesha ushirikiano wa hali ya juu kuwanusuru watu hao akiwemo mwanamke
mmoja,” alieleza.
Habari kwa hisani ya vyombo vya
habari.
No comments:
Post a Comment