Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza mfumuko wa bei wa Taifa wa mwezi
Novemba, 2017.
|
NA ISSA RAMADHANI,
MFUMUKO wa Bei wa Taifa wa mwezi Novemba, 2017 umepungua hadi
kufikia asilimia 4.4 kutoka asilimia 5.1 mwezi Oktoba, 2017.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam leo, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei
kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma
mbalimabli kwa mwezi Novemba, 2017.
“Mfumuko wa Bei wa
mwezi Novemba, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 4.4 kutoka asilimia 5.1 kwa
mwezi uliopita wa Octoba, 2017. Hii imechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi
ya bidhaa za vyakula kama vile nyama ya ngombe ambayo imepungua kwa asilimia
5.4, samaki wabichi kwa asilimia 22.2, mbogamboga kwa asilimia 3.9, viazi
mviringo kwa asilimia 14.0, mihogo mibichi kwa asilimia 24.8 na viazi vitamu
kwa asilimia 13.4,” amesema Kwesigabo.
Amesema fahirisi za bei zimeongezeka hadi
108.94 mwezi Novemba, 2017 kutoka 108.41 mwezi Oktoba, 2017.
Kwesigabo amesema mfumuko wa bei nchini
Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki
ambapo nchini Kenya Mfumuko wa Bei wa mwezi Novemba, 2017 umepungua hadi
asilimia 4.73 kutoka asilimia 5.72 mwezi Oktoba, 2017 na nchini Uganda
umepungua hadi asilimia 4.0 mwezi Novemba, 2017 kutoka asilimia 4.8 mwezi
Oktoba, 2017.
Amesema bidhaa zisizo za vyakula
zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei ni pamoja na mafuta ya taa
yaliyoongezeka kwa asilimia 4.6, mafuta ya dizeli kwa asilimia 2.0 na mafuta ya
petrol kwa asilimia 2.8.
Amesema uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania
katika kununua bidhaa na huduma umefikia Shilingi 91 na senti 79 mwezi Novemba,
2017 ikilinganishwa na Shilingi 92 na senti 25 ilivyokuwa mwezi Oktoba, 2017.
No comments:
Post a Comment