NA MWANDISHI WETU.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya
mazungumzo na Mabalozi wa Tanzania nchini Misri, Balozi Meja Jenerali Issa
Suleiman Nassoro na Balozi Abdulrahman Kaniki wa Zambia, ambapo amewataka
wakaimarishe mahusiano baina ya nchi zote mbili.
Amekutana na Mabalozi hao Balozi leo (Alhamisi,
Novemba 16, 2017) katika Ofisi ya Waziri Mkuu iliyopo Barabara ya Reli na
Mahakama mijini Dodoma na kuwasisitiza wakaboreshe shughuli za Kidiplomasia
kati ya Tanzania na nchi za Misri na Zambia.
Amesema licha ya kutangaza fursa za uwekezaji
na vivutio vya utalii pamoja na kuboresha biashara baina ya Tanzania na nchi za
Misri na Zambia pia wakawashawishi wawekezaji waje wawekeze katika sekta
mbalimbali nchini ikiwemo ya viwanda.
Waziri Mkuu amesema Tanzania ni nchi salama
yenye amani na utulivu wa kisiasa, pia Serikali imeweka mazingira mazuri ya
uwekezaji jambo ambalo litawawezesha wawekezaji watakaokuja kuwekeza nchini
kupata tija.
Pia Waziri Mkuu amewataka Mabalozi hao
wahakikishe wanakwenda kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa
nchini.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka Mabalozi hao
kwenda kukutana na kufanya mazungumzo na Watanzania waishio kwenye nchi hizo na
kuwasisitiza waishi kwa kuzingatia sheria za nchi husika. Pia wawaunganishe
pamoja na kuwashauri waje kuwekeza nchini.
Kwa upande wao Mabalozi hao wamesema watahakikisha
wanayafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa na Waziri Mkuu ikiwa ni pamoja na
kwenda kutafuta wawekezaji ili wawe kuwekeza katika sekta ya viwanda na
kuboresha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hizo.
No comments:
Post a Comment