NA MOHAMEDI NG`OULA
JUMUIYA ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi
(CCM), Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam, imewataka viongozi waliochaguliwa
hivi karibuni kuongoza jumuya hiyo kwa ngazi ya Matawi na Kata kuendana na kasi
ya mabadiliko ya chama hicho katika kuwajibika.
Katibu wa jumuiya hiyo wilayani ya
Kinondoni, Ibrahim Mpwapwa alitoa wito huo wakati wa semina elekezi na mafunzo
ya ujasiriamali kwa viongozi hao iliyofanyika katika ukumbi wa CCM Kata ya Kawe, Manispaa ya Kinondoni na kusema kuwa wakati umefika sasa kwa kila mwanachama kushindana katika fursa
mabalimbali za kiuchumi.
Akifafanua, Mpwapwa alisema mpango
wa jumuiya ya wazazi wilayani humo ni kuhakikisha kuwa kila kiongozi
anawajibika katika nafasi yake ikiwa ni pamoja na kupita kila Kata na Tawi
kuhamasisha wajibu wa jumuiya hiyo, kiuchumi, elimu, mazingira, malezi na
maadili kwa mujibu wa kanuni ya jumuiya hiyo.
Utendaji ni pamoja na kila kiongozi
kuzingatia maadili, bidii katika katika kazi na kufanya vikao kisha kupeleka
muhtasari ya vikao na mikutano kwenye ngazi husika, mathalani ngazi ya tawi
wanapaswa kupeleka Kata na hatimaye Wilayani.
Kwa kufanya hivyo alisema, watakuwa mfano na kivutio
kwa watu wanao waongoza na wengine ambao sio wanachama wa CCM au Jumuiya hiyo
kujiunga na chama hicho kwa yapo watu hao wanaojifunza kupitia kwao.
“Kiongozi asiyekwenda na wakati,
mvivu, mvunjifu wa maadili atambue kwamba ataondolewa kwenye nafasi yake. Tunataka
jumuiya ya wazai ya mfano, CCM yenye maendeleo. Lazima tufanya kazi kwa wito na
kwa maadili yenye mvuto,”alisisitiza Mpwapwa.
Sifa zingine za kiongozi wa
jumuiya hiyo ni kuwa wakati wote anabuni mbinu mbalimbali za kuhakikisha kwamba
chama chake kinashinda nafasi za uongozi, kuongeza wanachama na kubuni vyanzo
vya fedha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya
hiyo Kata ya Kawe, Benjamini Maliwa alisema
pamoja na majukumu kisiasa kwa viongozi hao, ni wajibu wao kuhakikisha kwamba
wanashiriki mafunzo ya kujiajiri ili kufikia malengo ya taifa la uchumi wa kati
ya njia ya viwanda.
“Tumekusudia kila mmoja wetu
anajishughulisha na ujasiriamali kwa wale ambao hawana vyanzo vingine vya
mapato kama vile ajira. Ili kufikia malengo hayo, ni lazima kuwapo kwa mafunzo
kama haya ambapo huweza kumfanya mtu kuwa na mfugaji, mkulima na hatimaye
kuanzisha kiwanda kidogo cha uchakataji wa mazao ngazi ya kaya au
kwingine,”alisema.
No comments:
Post a Comment