Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto)
akisalimiana na Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la Japan –JICA nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase, alioambatana
na Makamu wa Rais wa Shirika hilo Bw. Hiroshi Kato (katikati)
walipowasili katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es
Salaam.
NA MWANDISHI WENU.
SHIRIKA la Kimataifa la Maendeleo la
Japan (JICA) limesema liko tayari kushirikiana na Serikali kujenga
miundombinu ya kisasa ya usafiri, Nishati ya umeme, maji na usafi wa
mazingira katika Makao Makuu ya nchi, Dodoma.
Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa
Shirika hilo Bw. Hiroshi Kato wakati alipokutana na kufanya mazungumzo
na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Jijini Dar es Salaam.
Bw. Kato alisema kuwa mradi mwingine
wanaotaka kuutekeleza katika mji wa Dodoma ni udhibiti wa taka ngumu na
kwamba wanachosubiri ni Serikali kuainisha maeneo ya vipaumbele
vilivyoko katika mpango mji wa Dodoma.
Aidha Makamu
huyo wa Rais wa JICA alisema kuwa Shirika lake litaendelea kusaidia
eneo la kilimo hususan kilimo cha mpunga ili kuongeza thamani ya zao
hilo na kuwakomboa wakulima.
Wajumbe walioambatana na Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Hiroshi Kato wakifuatilia kwa makini
majadiliano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor
Mpango (Mb) (hayupo pichani) na mgeni wake ambaye ni Makamu wa Rais wa
JICA Bw. Hiroshi Kato, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango amelishukuru Shirika hilo kwa kuonesha nia ya kusaidia ujenzi wa
mji wa Dodoma ambao ndio Makao Makuu ya nchi.
Alisema kuwa mradi huo utasaidia kwa
kiasi kikubwa kuupanga mji wa Dodoma mapema ili kuondoa changamoto za
msongamano wa huduma za jamii kwenye eneo moja kama ilivyo Jijini Dar es
Salaam.
“Pamoja na umuhimu wa miundombinu ya
maji, umeme, usafiri wa mjini, lakini pia tunataka tujenge mapema njia
za juu (ring roads) ili kudhibiti msongamano wa magari” alisema Dkt.
Mpango.
Aliongeza kuwa mradi mwingine wa
kipaumbele katika mji huo ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa
katika eneo la Msalato, karibu kilometa 20 kutoka katikati ya mji huo
ili kurahisisha usafiri kwa njia ya anga.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), wa nne
kushoto na Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan
(JICA), Bw. Hiroshi Kato (wa tano kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja
na baadhi ya maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na
Serikali ya Japan, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini
Dar es Salaam. (Picha na Wizara ya Fedha na Mipango).
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika
zinazopata ufadhili mkubwa wa miradi mbalimbali ya maendeleo kutoka
Japan kupitia Shirika hilo la Kimataifa la Maendeleo (JICA).
Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa
barabara ya juu (fly over) katika eneo la Tazara Jijini Dar es Salaam,
upanuzi wa awamu ya kwanza ya barabara mpya ya Bagamoyo (Mwenge-Tegeta)
na ufadhili mpya wa awamu ya pili ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka
Morocco hadi Mwenge.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na
Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la
Japan (JICA) nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase, pamoja na Maafisa
waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Mamlaka ya Mapato
Tanzania TRA.



No comments:
Post a Comment