JESHI la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania
limesema kikundi chake cha ulinzi na usalama kilichopo DRC kwaajili ya kutekeleza
jukumu la ulinzi na amani kilivamiwa na Waasi waliojilikana kuwa ni ADF na
kusababisha mauaji kwa wanajeshi 14.
Amesema kwamba tukio hilo lilitokea katika eneo la kambi iliyopo
daraja kwenye mto Simulike barabara ya kutokea Oicha kwenda Kamango mpakani mwa
nchi ya Uganda Kaskazini Mashariki ya wilaya ya Beni Jimbo la Kivu Kaskazini.
Akithibitisha mauaji hayo muwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi na Usalama Tanzania (CDF) Luteni Jenerali James Mwakibolwa amesema
shambulio hilo lakuvamiwa lilizusha mapigano baina ya kikundi hicho na kile cha
waasi na yalidumu kwa takribani masaa kumi na tatu (13) na kusababisha vifo vya
askari wa Tanzania 14 na wengine 44 kujeruhiwa na askari wawili bado
hawajulikani walipo ambapo jitihada zaidi za kuwatafuta zinaendelea.
Amesema shambulizi la tarehe 7 kuamkia tarehe 8 Desemba lilikua
baya zaidi kuwahi kuitokea tangu vikosi hivyo vianze kushiriki ulinzi wa amani
nchini DRC mwaka 2011 kwakua limeleta madhara makubwa, hata hivyo kikundi hicho
ambacho bado kipo huko kinauwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu husika kwa
uhodari wa hali ya juu ,ushupavu, weledi mkubwa na umahiri stahiki.
Kwa niaba ya mkuu wa majeshi Luteni Jenerali Mwakibolwa
amewathibitishia watanzania kuwa tukio hilo halitawavunja moyo na kamwe Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania halitatetereka kupeperusha bendera yake ndani
na nje ya nchi kwani tukio hilo limewaongezea nguvu, ari ,ushupavu na uhodari
zaidi katika kutekeleza majukumu yake.
Aidha amesema nchi pia iko salama na itaendelea kuwa salama na
yeyote ambaye anataka kuwajaribu atashughulikiwa ipasavyo kwani historia ya
jeshi inadhihirisha uwezo thabiti.
Kuhusu taratibu za kusafirisha miili ya marehemu kuirejesha
nchini zinafanyika chini ya utaratibu wa Serikali na umoja wa mataifa na JWTZ
na serikali wanaendelea kuchukua hatua stahiki kufuatia tukio hilo ikiwemo
kufanya uchunguzi katika eneo husika sambamba na kuangalia taratibu za
kuwajulisha familia za wafiwa zimekamilika na ndio maana hawakuweza kutoa
taarifa hizo bila kuwaweka sawa familia za mashujaa hao.
Kwa umoja wa watanzania amewataka kuwaombea dua roho za mashujaa
hao zipumzike mahali pema peponi kwa amani na majeruhi wote wapone haraka
iwezekanavyo ili warejee kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa ulinzi wa
taifa na dunia nzima.
No comments:
Post a Comment