Rais Uhuru Kenyatta akiwa na mwanafunzi bora
kitaifa, Goldalyn Kakuya
KENYA,Nairobi
MSICHANA mwenye ulemavu wa ngozi (albino) amesema ushindi wake wa kuwa
namba moja kitaifa kwenye mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya msingi nchini
Kenya (KCPE) ni ushindi wa albino wote na kwamba, hakuna anayeweza kutimiza
ndoto zake bila alichoiita kuwa ni Ph.D yaani sala, juhudi na nidhamu.
Kwa mujibu wa matokeo
yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu Kenya, mtoto huyo, Goldalyn Kakuya (14)
amepata maksi 455 kati ya 500. Wanafunzi 993,718 walifanya mtihani huo. Mwaka
jana mwanafunzi wa kwanza kitaifa alipata maksi 437.
Mbunge wa Kuteuliwa,
Dk David Sankok aliwapongeza wanafunzi sita wenye ulemavu kwa kuwa miongoni mwa
watahiniwa 100 bora kitaifa. “Leo sitaki tusheherekee kwa ajili yangu tu,
nataka tusheherekee ualbino,” alisema Goldalyn.
Ijumaa iliyopita
msichana huyo aliyekuwa akisoma kwenye Shule ya Mtakatifu Anne Junior iliyopo
Lubao kwenye jimbo la Kakamega, alikwenda Ikulu ya Kenya kukutana na Rais
Mteule, Uhuru Kenyatta na Naibu Rais mteule, William Ruto.
Kenyatta na Ruto
walimpongeza Goldalyn kwa mafanikio aliyopata. Kenyatta aliahidi kumsaidia
mtoto huyo atimize ndoto zake. Wakati akiwa hapo Ikulu na wazazi wake, msichana
huyo alipata fursa ya kuzungumza na Rais Kenyatta na kumkumbatia kiongozi huyo.
“Nilimpongeza na
nilizungumza na mwanafunzi bora wa mwaka huu KCPE Goldalyn Kakuya. Goldalyn ana
mwelekeo mzuri sana wa maisha yake ya baadaye na utawala wetu utahakikisha
kwamba anapata kila aina ya msaada anaohitaji kutimiza ndoto zake,” alisema.
Katika hafla hiyo,
wazazi wa msichana huyo walikabidhiwa hundi ya Shilingi 100,000 za Kenya. Mama
mzazi wa msichana huyo, Matilda Tanga, alisema alifahamu binti yake angefanya
vizuri kwenye mtihani huo, lakini hakutarajia kuwa angekuwa wa kwanza kitaifa.
“Goldalyn ametuma
ujumbe kwa watu wanaowadharau watoto wenye ulemavu wa ngozi, na amethibitisha
kwamba mtoto mwenye ualbino akipata upendo na kupewa fursa wanaweza kuufikia
uwezo wao,” alisema. Baba mzazi wa Goldalyn, Harrison Tanga, anaikumbuka siku
aliyozaliwa mtoto huyo, Aprili 20, 2003.
“Nilipomwona
(Goldalyn) nilimkumbatia mke wangu, Goldalyn ni dhahabu yangu,” alisema Tanga.
Wakati wa sherehe ya kumpongeza iliyoandaliwa na Jumuiya ya Wenye Ualbino
nchini Kenya, Goldalyn alisema alichofanyiwa ni ujumbe kwa jamii kusheherekea
ualbino na watu wenye ulemavu huo.
“Tunaweza kuwa
vyovyote tunavyotaka,” alisema msichana huyo kwenye sherehe hiyo katika ofisi
za ASK, Nairobi. Alitoa mwito kwa wanafunzi wenye ualbino kusoma kwa bidii.
“Huwezi kutimiza ndoto zako bila PhD: sala, juhudi na nidhamu,” alisema mtoto
huyo.
Kwa mujibu wa
Goldalyn, siku za nyuma alikuwa akikaa ndani tu ili watu wasimwone, lakini
akapata hali ya kujiamini na kwamba kwa sasa hajisikii vibaya kuwa na ulemavu
wa ngozi. Waziri wa Elimu, Dk. Fred Matiang’i alitangaza matokeo siku 19 tu
baada ya kumalizika kwa mtihani huo, uliofanywa kuanzia Oktoba 31 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Baraza
la Taifa la Mitihani Kenya (KNEC), matokeo yamewahi kutolewa kwa sababu
mchakato wa kusahihisha, uliharakishwa kwa kutumia mashine ziitwazo automated
Optical Mark Recognition Katika matokeo hayo, wanafunzi 9,846 walifanikiwa
kupata zaidi ya maksi 400.
Matiang’i alisema,
watahiniwa wote kutoka shule za serikali na binafsi, waliopata zaidi ya maksi
400 watapelekwa kusoma kwenye shule za sekondari za serikali. Wanafunzi sita
kutoka shule zenye mahitaji maalumu, wamekuwa miongoni mwa watahiniwa 100 bora.
Watahiniwa 2,360 walipata maksi chini ya 100.
Mchakato wa kuchagua
watakaojiunga na kidato cha kwanza, unatarajiwa kuanza Desemba nne na kazi ya
kuwapangia shule itakuwa imekamilika ifikapo Desemba 12. Matiang’i
alifurahishwa na matokeo ya shule za serikali. Alisema mwanafunzi wa pili kwa
ubora kitaifa, ametoka shule ya serikali ya bweni, Kathigiri na amepata maksi
447.
Alisema, mwanafunzi
bora kutoka shule za wenye mahitaji maalumu amepata maksi 426. Kwa ujumla,
watahiniwa sita kutoka shule hizo wamepata maksi zaidi ya 400. Kwa mujibu wa
Matiang’i watahiniwa kwenye mtihani huo, hawakufanya vizuri kwenye sayansi na
masomo maalum.
Rais mteule wa Kenya,
Uhuru Kenyatta alimuagiza Waziri wa Elimu wa nchi hiyo, Dk Fred Matiang’i
wanafunzi ambao hakuwafanya mtihani KCPE kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo
ya kufiwa, ugonjwa au kujifungua, wapewe wafanye.
Alitoa agizo hilo
alipozungumza na Matiang’i kwenye ofisi za Kenyatta katika jengo la Harambee
kabla ya kutolewa kwa matokeo ya mtihani huo Msemaji wa Ikulu ya Kenya, Manoah
Esipisu, alisema, katika mazungumzo ya Rais Kenyatta na Dk Matiang’i, kiongozi
huyo wa nchi alisema, wanafunzi ambao hawakufanya mtihani huo kwa sababu zenye
mantiki wakiwemo waliokuwa wamefiwa na wazazi, waliojifungua na waliokuwa
wagonjwa, wapewe mtihani na kwamba, utaratibu kama huo unafanyika sehemu nyingi
duniani
|
No comments:
Post a Comment