| Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza |
NA
MWANDISHI WETU,
MAZUNGUMZO
kuhusu mgogoro wa kisiasa Burundi,
yanatarajiwa kufanyika nchiya Tanzania kwa siku 13 kuanzia wiki hii jijini
Arusha, chini ya Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Tanzania, Benjamin
Mkapa.
Hayo yamethibitishwa na Mkapa, ambaye ni
mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) aliyekabidhiwa jukumu la
Burundi. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mawasiliano kwenye
Sekretarieti ya EAC, Richard Owora Othieno, mazungumzo hayo yanatarajiwa kuwa
na maamuzi muhimu.
Hata hivyo, bado haijaelezwa wazi ajenda
hasa za mazungumzo yajayo na hata pande zitakazoshirikishwa katika mazungumzo
hayo. Serikali ya Burundi ilikataa kushiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja
na upinzani, ikiutuhumu kwamba ulihusika katika jaribio la mapinduzi yaliyofeli
ya Mei mwaka 2015.
Kihistoria nchi ya Burundi iliingia katika
machafuko Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD, kumuidhinisha
Pierre Nkurunziza kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu uliopita, ikiwa ni
kwa mara ya tatu mfululizo.
Wapinzani wa kisiasa waliitaja hatua ya
Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba ilikiuka Katiba na hati ya
Makubaliano ya Amani ya Arusha, lakini Serikali ya Burundi ilisisitiza kwamba
haijakiuka sheria.
No comments:
Post a Comment